Tuesday, July 26, 2011

HISTORIA YA CHUO:


Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kina historia ndefu yenye umri sawa na uhuru wa Tanzania Bara. Ni vigumu kuzungumzia Uhuru wa Tanzania bila kukihusisha Chuo cha Kivukoni (Sasa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere), kwani Chuo hiki kilianzishwa kwa lengo la kuwaandaa Watanganyika kushika madaraka baada ya Uhuru.
Chuo hiki kimepitia mifumo mitatu tofauti kabla ya kuitwa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

1961 – 1971: Chuo cha Kivukoni ( Kivukoni College)
Chuo kilianzishwa tarehe 29 Julai, 1961 na kufunguliwa rasmi na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika, Mheshimiwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Chuo kilisajiliwa rasmi tarehe 05 Desemba, 1961. Siku nne kabla ya Tanganyika kupata Uhuru.
Chuo kilianza na Wanafunzi 43 ambao walikuwa wakisoma Siasa, Historia, Uongozi, Sheria, Elimu ya Jamii, Fasihi, Jiografia, Lugha pamoja na masomo mengine.
• Chuo kilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni (Sura 212). Wamiliki wa Chuo kwa mujibu wa “Memorandum and Articles of Association of Kivukoni College” walikuwa wanne:
(a) The Tanganyika Education Trust Fund (TETF).
(b) The Tanganyika African National Union (TANU).
(c) The Co-operative Union of Tanganyika (CUT) na
(d) The Tanganyika Federation of Labour (TFL).
• Chuo kilipewa jina la Kivukoni ikiwa ina maana mbili:
Kwanza kuja Chuoni mwanafunzi analazimika kuvuka bahari kwa kivuko, pili kwa kupitia mafunzo, mwanafunzi anakuwa amevuka kielimu na kisaikolojia.
Jengo hili la Uhuru ndilo Jengo la kwanza kutumika kufundishia wanafunzi wa Chuo cha Kivukoni, Julai 1961. Jengo hili hivi sasa lina vyumba vya madarasa, ofisi za wafanyakazi, maabara za Kompyuta pamoja na kumbi za mikutano.

1971 - 1992 Chuo Cha Chama Kivukoni (Kivukoni Ideological College) -.


 Mwaka 1971, Chama Cha Mapinduzi kilianzisha rasmi Sera ya Chama Kushika Hatamu. Kwa mujibu wa sera hii, Chama ndicho kilikuwa na nguvu, mamlaka na madaraka kuliko chombo kingine chochote nchini. Katika kutekeleza sera hiyo, Kivukoni College kililazimika kufanya mageuzi bila ya mabadiliko ya kisheria.
Jina la Chuo lilibadilika na kuwa Chuo cha Chama Kivukoni (Kivukoni Ideological College).
Jukumu kuu la Chuo lilikuwa kufundisha Itikadi ya Chama ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa viongozi wa Chama, Serikali na Mashirika ya Umma, Kufanya Utafiti na kutoa ushauri kwa Chama. 

1992 hadi Septemba, 2005 - Cho cha Sayansi Jamii Kivukoni (Kivukoni Academy of Social Sciences)


Nchi yetu ilirejea rasmi kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa kuanzia tarehe 1 Julai, 1992.
Chuo cha Chama Kivukoni kililazimika kufanya mageuzi ambayo yangeendana na mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Chuo zilikuwa zifuatazo:- 3 50th Anniversary

(1) Kusajili upya Chuo chini ya Sheria ya Makampuni (Sura 212) tarehe 20 Novemba, 1992.
(2) Chuo kilitambulika rasmi kwa jina la Chuo cha Sayansi Jamii Kivukoni (Kivukoni Academy of Social Sciences).
(3) Vyuo vyote vya Kanda, isipokuwa Chuo cha Kanda cha Zanzibar, vilifungwa. Chuo cha Lushoto kiliuzwa kwa Idara ya Mahakama, Chuo cha Kihinga kiliuzwa kwa Kanisa Katoliki, Jimbo la Kigoma na Vyuo vingine vitano vilivyobaki vilikabidhiwa Serikalini.
(4) Majukumu makuu ya Chuo yalibadilika. Chuo kilikuwa na majukumu yafuatayo:-
(a) Kufundisha taaluma katika Sayansi Jamii, hususan programu za mafunzo zifuatazo:-
• Stashahada katika Sayansi Jamii (Diploma in Social Sciences)
• Stashahada katika Maendeleo ya Uchumi (Diploma in Economic Development)
• Stashahada ya Masuala ya Jinsia katika Maendeleo (Diploma in Gender Issues in Development)
• Cheti katika Kazi za Vijana (Certificate in Youth Work).
(b) Kufanya tafiti katika masuala ya Sayansi Jamii na
(c) Kutoa ushauri wa kitaalamu kwa sekta ya umma na sekta binafsi. 4 50th Anniversary 

MABADILIKO TOKA CHUO CHA SAYANSI JAMII KIVUKONI KWENDA CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE


Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilianzishwa kwa Sheria Namba 6 ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 2005 na kutoka katika gazeti la Serikali Namba 433 la tarehe 23 Desemba, 2005. Sheria hii ilianza kutumika rasmi tarehe 01 Oktoba, 2005.
Chimbuko la kuanzisha Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni mafanikio yaliyopatikana kutokana na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES). Mafanikio hayo yalisababisha Serikali kufungua milango zaidi ya elimu ya juu hivyo kuongeza idadi ya vyuo vya elimu ya juu vya binafsi na vya umma.
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilirithi shughuli, mali, madeni, wafanyakazi na wanachuo wa kilichokuwa Chuo cha Sayansi Jamii Kivukoni ambacho uhai wake ulikoma rasmi tarehe 30 Septemba, 2005.
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kinamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizarayenye dhamana ya Elimu.
Kwa mujibu wa kifungu 4 (1) cha Sheria Namba 6 ya 2005 ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, majukumu makuu ya Chuo ni pamoja na yafuatayo:
(a) Kutoa mafunzo katika fani za Sayansi Jamii kwa kiwango cha Cheti, Stashahara na Shahada.
(b) Kutoa mafunzo ya Uongozi (leadership).
(c) Kuendesha mafunzo ya Elimu ya Kujiendeleza (Continuing Education).
(d) Kufanya utafiti.
(e) Kutoa ushauri wa kitaalamu kwa sekta ya umma na sekta binafsi.
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilirithi Usajili kamili (Full Registration) wa Chuo cha Sayansi Jamii Kivukoni uliopatikana Mei, 2002. Aidha, Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilipata Ithibati Kamili (Full Accreditation) Novemba, 2005. Usajili Kamili na Ithibati Kamili vilitolewa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa mujibu wa Sheria Na. 9 ya 1997.
Chuo hiki kimepewa jina la Mwalimu Nyerere kwa lengo la kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa ambaye alifanya kazi kubwa ya ukombozi wa Taifa letu, ukombozi wa Bara la Afrika na kuwatetea wanyonge popote duniani.