Tuesday, July 26, 2011

HISTORIA YA CHUO:


Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kina historia ndefu yenye umri sawa na uhuru wa Tanzania Bara. Ni vigumu kuzungumzia Uhuru wa Tanzania bila kukihusisha Chuo cha Kivukoni (Sasa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere), kwani Chuo hiki kilianzishwa kwa lengo la kuwaandaa Watanganyika kushika madaraka baada ya Uhuru.
Chuo hiki kimepitia mifumo mitatu tofauti kabla ya kuitwa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

1961 – 1971: Chuo cha Kivukoni ( Kivukoni College)
Chuo kilianzishwa tarehe 29 Julai, 1961 na kufunguliwa rasmi na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika, Mheshimiwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Chuo kilisajiliwa rasmi tarehe 05 Desemba, 1961. Siku nne kabla ya Tanganyika kupata Uhuru.
Chuo kilianza na Wanafunzi 43 ambao walikuwa wakisoma Siasa, Historia, Uongozi, Sheria, Elimu ya Jamii, Fasihi, Jiografia, Lugha pamoja na masomo mengine.
• Chuo kilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni (Sura 212). Wamiliki wa Chuo kwa mujibu wa “Memorandum and Articles of Association of Kivukoni College” walikuwa wanne:
(a) The Tanganyika Education Trust Fund (TETF).
(b) The Tanganyika African National Union (TANU).
(c) The Co-operative Union of Tanganyika (CUT) na
(d) The Tanganyika Federation of Labour (TFL).
• Chuo kilipewa jina la Kivukoni ikiwa ina maana mbili:
Kwanza kuja Chuoni mwanafunzi analazimika kuvuka bahari kwa kivuko, pili kwa kupitia mafunzo, mwanafunzi anakuwa amevuka kielimu na kisaikolojia.
Jengo hili la Uhuru ndilo Jengo la kwanza kutumika kufundishia wanafunzi wa Chuo cha Kivukoni, Julai 1961. Jengo hili hivi sasa lina vyumba vya madarasa, ofisi za wafanyakazi, maabara za Kompyuta pamoja na kumbi za mikutano.

No comments:

Post a Comment