Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilianzishwa kwa Sheria Namba 6 ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 2005 na kutoka katika gazeti la Serikali Namba 433 la tarehe 23 Desemba, 2005. Sheria hii ilianza kutumika rasmi tarehe 01 Oktoba, 2005.
Chimbuko la kuanzisha Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni mafanikio yaliyopatikana kutokana na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES). Mafanikio hayo yalisababisha Serikali kufungua milango zaidi ya elimu ya juu hivyo kuongeza idadi ya vyuo vya elimu ya juu vya binafsi na vya umma.
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilirithi shughuli, mali, madeni, wafanyakazi na wanachuo wa kilichokuwa Chuo cha Sayansi Jamii Kivukoni ambacho uhai wake ulikoma rasmi tarehe 30 Septemba, 2005.
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kinamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizarayenye dhamana ya Elimu.
Kwa mujibu wa kifungu 4 (1) cha Sheria Namba 6 ya 2005 ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, majukumu makuu ya Chuo ni pamoja na yafuatayo:
(a) Kutoa mafunzo katika fani za Sayansi Jamii kwa kiwango cha Cheti, Stashahara na Shahada.
(b) Kutoa mafunzo ya Uongozi (leadership).
(c) Kuendesha mafunzo ya Elimu ya Kujiendeleza (Continuing Education).
(d) Kufanya utafiti.
(e) Kutoa ushauri wa kitaalamu kwa sekta ya umma na sekta binafsi.
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilirithi Usajili kamili (Full Registration) wa Chuo cha Sayansi Jamii Kivukoni uliopatikana Mei, 2002. Aidha, Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilipata Ithibati Kamili (Full Accreditation) Novemba, 2005. Usajili Kamili na Ithibati Kamili vilitolewa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kwa mujibu wa Sheria Na. 9 ya 1997.
Chuo hiki kimepewa jina la Mwalimu Nyerere kwa lengo la kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa ambaye alifanya kazi kubwa ya ukombozi wa Taifa letu, ukombozi wa Bara la Afrika na kuwatetea wanyonge popote duniani.
No comments:
Post a Comment